15 Machi 2011

Diamond 'alitifua' Tuzo za Injili

Diamond Tanzania

MSANII wa muziki wa kizazi kipya ‘Bongo Fleva’ Nassib Abdul ‘Diamond’, juzi alisababisha mtafaruku baada ya mashabiki kuacha kufuatilia Tuzo za Injili na kubaki wakimshangilia kwa kupiga kelele za shangwe.

Diamond aliingia katika Ukumbi wa Diamond Jubilee zilipokuwa zikiendelea shughuli za utoaji tuzo hizo majira ya saa 10 jioni, huku akiwa na wapambe akiongozwa mwanadada mmoja ambaye hakufahamika jina lake mara moja na kuelekea katika meza aliyokuwa amekaa mchekeshaji wa kundi la Komedi, Masanja Mkandamizaji.

Mara baada ya kukaa huku akifuatilia kwa makini uimbaji wa mwimbaji wa muziki wa injili, Sara Mvungi, aliyekuwa akiimba wakati huo, ndipo kamera zilizokuwa katika ukumbi huo zilimnasa na kumvuta kwa ukaribu, hali iliyowafanya mashabiki waliokuwa wameelekeza macho yao jukwaani kuacha na kuelekeza katika ‘Screen’ zilizokuwapo ukumbini na kuanza kunyoosha vidole kuelekeza katika picha hiyo ya Diamond.

Tukio hilo lilidumu kwa takriban dakika tano kabla ya kurejea hali ya kawaida, huku Diamond mwenyewe akilazimika kushika kichwa kama ishara ya kuonyesha kushangaa kitendo hicho cha kushangiliwa.

Mbali na Diamond, wengine waliohudhuria tamasha hilo ni pamoja na Mwasiti, Vicky Kamata na Linah wa THT.

Katika tuzo hizo, ilishuhudiwa waimbaji wakongwe wakibwaga na vijana wakiwamo Florah Mbasha, Bahati Bukuku na Rose Muhando ambao hawakuambulia kitu.

Mwimbaji Martha Mwaipaja aliibuka na tuzo ya msanii bora mpya wa kike, Miriam Shilwa ambaye ni mlemavu wa macho, aliibuka mshindi na tuzo ya balozi bora wa jamii baada ya kuwabwaga wakongwe ambao ni Flora Mbasha, Christina Shusho na Ambwene Mwasongwe waliokuwa wakiwania katika kundi hilo.

Mwimbaji Christina Shusho alishinda tuzo ya msanii bora wa kike wa jumla wa mwaka huku Bonny Mwaitege akiibuka na tuzo ya msanii bora wa kiume kwa albamu yake inayojulikana kama ‘Mama’.