Jina la Usajili:  Neno la Siri:    Umesahau neno la siri?   |   Umesahau jina?
01 Julai 2011

Msanii, Heshima huanza na Wewe

Msanii, Heshima huanza na Wewe

KWA yakini nisingelazimika kuandika mtazamo huu kama nisingetokewa na jambo hili ninalotaka kulielezea hapa chini.

Jumanne iliyopita niliwatembelea mazoezini kwao wasanii wa kundi jipya la mipasho; Kings Modern Taarab, Mburahati, jijini Dar es Salaam katika pilikapilika zangu za kawaida kama mwandishi.

Cha kusikitisha na kukatisha tamaa, ukiondoa Mkurugenzi Mkuu wa kundi hilo, Hamis Majaliwa, pamoja na wasanii wachache wanaojua umuhimu wa
vyombo vya habari, sikupata kabisa ushirikiano kwa wengine waliobakia.

Nilipofika eneo lile la mazoezi ambako ni kwenye ukumbi wa Kings Park, Mburahati, wasanii wale walionyesha kujiona wao ndio wao, hasa baada ya kutambulishwa kuwa mimi ni mwandishi wa habari.

Bila kuzingatia kuwa lengo langu kwao lilikuwa ni kuwatangaza na kuwafanya wajulikane kwa mashabiki wa mipasho, walianza kunidharau na kila niliyemuuliza lolote alijibu alivyojisikia mwenyewe.

Hiyo haikuwa kero kubwa kwangu, kutokana na kwamba nafahamu hulka za wasanii wengi ni wenye majivuno, ila kilichonichoma zaidi ni mmoja wa wasanii wa kundi hilo kutamka wazi eti ninawazingua.

“We nani kwetu na umefuata nini hapa, sisi hatuhitaji msaada wako bwana, afadhali ungekuwa ‘Dida’ au ‘Mishi’, lakini si magazeti,” alisema msanii yule niliyemfahamu baadaye kuwa anaitwa Ally Besi.

Nakumbuka alisema mengi msanii yule ambaye nafasi yake ndani ya Kings ni kusaidia kupiga gitaa la besi  pindi mpigaji mkuu wa chombo hicho, Hamad Bass,  anapochoka.

Bila kuficha kitu, kutokana na mapokezi na kauli zile za baadhi ya wasanii wa Kings, nikajikuta napata la kuzungumza katika makala hii siku ya leo kuhusiana na wasanii wetu.

Kwakuwa ni desturi mbaya ambayo inaonekana kuchipua na kuota mizizi kwa kasi kwa wasanii wengi kudharau waandishi pamoja na vyombo vyao vya habari.

Wengine wao ndio kama hivyo, huwagawa waandishi na kwa kuweka matabaka ya vyombo wanavyoviona ndivyo vya kuvipapatikia na vingine vyote kuvipuuza.

Kimsingi hali hii ni mbaya kwa wasanii wenyewe, kwa kuwa wao hawawezi kutambua chombo kinachowapa kipaumbele zaidi ama kinachoweza kuwasaidia.

Aidha, ni mbaya zaidi kwa sababu, kama ilivyo kwa mwanadamu mwingine yeyote, pia mwandishi anapobaini kuwa msanii fulani anamdharau, hutokea kumchukia  na kuchukia kazi zake zote hata kama zina ubora uliopitiliza.

Visasi baina ya mwandishi na msanii husika vinaposhamiri, kuna hatari ya kuzuka bifu la chini kwa chini, ambalo matokeo yake ni kupondwa kwa kila kazi inayofanywa na msanii huyo.

Aidha, kama ilivyo aina ya sumu zote, chuki huweza kusambaa hata kuambukizwa waandishi na vyombo vingine vya habari kiasi cha kujikuta
msanii akididimia na kupotea kabisa kwa kukosa sapoti ya uhakika.

Ingawa kwa upande mwingine wasanii wa aina hii huwatia hasara wamiliki wa makundi yao, lakini zaidi ni kujizorotesha wao wenyewe, kwa sababu bosi anapoona kuwa huna tija kwake atakutimua na kuajiri mwingine.

Maoni yangu ni kuwa, huu ni wakati wa wasanii wote kubadilika na kuachana na kasumba za kishamba za majivuno na kudharau watu ambao ni nguzo kuu ya mafanikio yao.

Kwasababu naamini kuwa kama si jitihada za dhati za waandishi wa habari, hakuna hata msanii mmoja ambaye angeweza kusimama na kutamba kwenye gemu zaidi ya miaka miwili.

Hii ndiyo sababu inayowafanya hata wakongwe wetu wa muziki, pamoja na kujulikana kwao hata nje ya taifa letu, bado wanawathamini vilivyo waandishi wa habari na vyombo vyao.

Unafikiri kulikuwa na haja ya wakongwe wa muziki wenye majina makubwa hapa nchini kuendelea kuwanyenyekea waandishi kwa kuwakumbatia na kuwa tayari kuwapa ushirikiano wakati wowote?

Wangeringa wakongwe wa dansi kama Said Mabera, Shaaban Dede, Hussein Jumbe, Mafumu Bilali, Shem kalenga, Hassan Bitchuka, Muhidin Gurumo, Hamza kalala, Zahir Ally ‘Zorro’ na Tshimanga Kalala Asosa.

Kwenye muziki wa Kizazi Kipya ‘Bongo Fleva’ wangeringa wasanii kama Joseph Mbilinyi ‘Mr II’, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’, Joseph Haule ‘Profesa Jay’, Juma Kassim Kiroboto ‘Nature’ na Said Fella.

Ama katika hiyo mipasho, majivuno yangewatawala kina Fatma Baraka ‘Bi. Kidude’, Mohammed Elias, Khadija Kopa, Haji Mohammed, Mwanahela Salum, Patricia Hilary, Shakila said, Mwanahawa Ally na Mzee Yussuf na Ally Star?

Wao tayari ni maarufu, na unapotaja majina yao, anga ya muziki wa mipasho hutetemeka, lakini kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari, hawawadharau waandishi.

Bila shaka huu ni ulimbukeni tu wa baadhi ya wasanii wapya, ambao baada ya kuanza kuingia studio na kushiriki kurekodi nyimbo zinazotamba, huanza kuvimba vichwa na kujiona wao ni zaidi.

Habari na Abdallah Mensah

Login to post comments

MSANII WA WIKI

Loveness

MUIGIZAJI na Mtayarishaji wa Filamu Tanzania Loveness Watson Nyota yake kwa sasa inatingisha katika tasnia ya

Soma Zaidi...

VIDEO YA MHARIRI

Off Side

Si mara ya kwanza kutazama filamu za Kanumba, lakini pia ni ukweli kwamba kila filamu anayokuja nayo

Soma Zaidi...

FILAMU ZA BONGO

Mbawa za Dino Zafunguka

MUIGIZAJI na Mtayarishaji wa filamu hapa nchini Tanzania Dennis Sweya (Dino) anatarajia kuanza kurekodi

Soma Zaidi...

WAHAPAHAPA VIDEO

You need Flash player 6+ and JavaScript enabled to view this video.