04 Julai 2011

Vicky Aivalia Njuga Studio ya JK

Vicky Aivalia Njuga Studio ya JK

Baada ya Mbunge wa Mbeya Mjini,Joseph Mbilinyi (Chadema) kulalamika weeee kuhusu ile studio ya JK aliyotoa zawadi kwa wasanii,jana ilikuwa ni zamu ya mbunge wa Viti Maalum (CCM) Vicky Kamata.

Kamata ambaye pia ni msanii ameitaka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuwaeleza wasanii studio aliyotoa Rais Kikwete kwa ajili ya wasanii iko wapi.

Akichangia mjengoni (Bungeni) bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kamata alisema kwa kuzingatia umuhimu wa wasanii na sanaa, JK alitoa zawadi ya studio, lakini hadi leo haijulikani iko wapi na inawasaidia kina nani, ikiwa wasanii wenyewe wanahangaika.

Alisema, wakati umefika kwa wizara husika, kutoa ufafanuzi kama hiyo studio ililetwa zawadi kwa wasanii wote au ililetwa kwa ajili ya kumnufaisha mtu mmoja kwa manufaa yake binafsi.

Mbunge huyo, alisema, wanatakiwa kuelezwa pia ni utaratibu upi, kama studio hiyo iko wazi kwa wasanii, ambao utatumika katika kurekodi nyimbo zao kama Rais alivyoagiza.

“Rais wetu ametupatia studio kama zawadi kwa kila msanii, lakini nashangaa studio hiyo inakuwaje inakuwa mikononi mwa watu wachache na kupoteza lengo la Rais ambaye alitupenda na kutuzawadia... tunatakiwa kuelezwa na wizara husika, inatakiwa kutupa jibu juu ya hilo,” alisisitiza Kamata.

Habari na DHW