Jina la Usajili:  Neno la Siri:    Umesahau neno la siri?   |   Umesahau jina?
08 Julai 2011

Choki Unachemkia Padogo Kinoma - Mensah

Choki Unachemkia Padogo Kinoma - Mensah

HABARI za Sabasaba wadau wangu wa Kijiwe hiki cha burudani? Sina shaka mu wazima wa afya na mmetulia tulii majumbani kwenu mkiifurahia
sikukuu hii muhimu.

Kwa wale wenzangu na mimi, wafanyabiashara pamoja na baadhi ya wafanyakazi ambao hamna mapumziko ya wikiendi wala sikukuu, naamini muda huu mnapoendelea vema na pilikapilika za majukumu yenu ya kila siku.

Leo katika safu hii, nimeamua kumgeukia swahiba wangu wa siku nyingi, nguli wa uimbaji na Kiongozi wa bendi ya muziki wa dansi, Extra Bongo ‘Wana Next Level’, Ally Choki ‘Mzee wa Farasi’.

Nimeona iko haja ya kusema na Choki kuhusiana na hili nililoliona katika bendi yake hiyo, hasa kutokana na kuvutiwa mno na jitihada zake za kuhakikisha bendi hiyo inakuwa juu zaidi ya ilipo sasa.

Nilishasema sana huko nyuma, kuwa Choki akiamua anaweza, kwasababu namfahamu kijana mwenzangu huyu kuanzia vipaji alivyonavyo vya utunzi na uimbaji hadi ujasiri wake wa kupambana na kutokata tamaa katika gemu la muziki.

Kiukweli, Choki ni kati ya watu ambao katika sekta ya muziki binafsi napenda kuwaita ‘wabishi’, hasa kutokana na namna walivyokuwa tayari kwa lolote lile ilimradi tu wahakikishe lao linatimia.

Hakuna asiyefahamu kuwa Extra Bongo hii iliyopo sasa ni ufufuo baada ya ile iliyoanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 2004 na kufa muda mfupi baadaye huku ikituacha mashabiki tukiwa na kiu nayo.

Tangu ilipofufuliwa upya awamu hii ya pili, kiukweli Extra Bongo inaonekana bado ‘haijatulia kivile’ na kufikia kiwango kile cha awali wakati ilipokuwa kwenye chati kabla haijasambaratika, licha ya jitihada nyingi kufanywa.

Moja ya jitihada hizo ambazo mimi nikiwa mdau mkubwa wa muziki na sanaa kwa ujumla naziunga mkono, ni kuongezwa kwa wanamuziki kila pale inapoonekana kuwa inahitajika kufanya hivyo.

Lakini anapokosea Choki ni pale anaposhindwa kujua wanamuziki ambao ndio hitaji la kweli la mashabiki wake na ambao iwapo atafanya juu chini kuwapata na kuwasogeza kundini kwake, mambo yanaweza kuwa safi.

Kwasababu tumeshuhudia mara kadhaa akipora wasanii kutoka kundi fulani na kuwaleta Extra Bongo huku Extra Bongo hiyo ikiendelea kuwa bado iko palepale na wakati mwingine ikionekana kupungua makali.

Katika hili, nafikiri rafiki yangu Choki alipaswa kwanza kuzingatia kuwa, mabosi wake wakuu, kwa mana ya mashabiki, ni watu wa rika la kati, hususan masistaduu pamoja na mabrazamen ambao siku hizi wanajiita ‘Masharobaro’.

Ingawa tuko pia kina sisi ambao tayari umri umeshaanza kututupa mkono, lakini hao masharobaro na masistaduu ndio angewaweka mbele kwanza.

Kwakuwa wao kutokana na rika lao la ujana kuwaruhusu ‘kujirusha’ pamoja na kutobanwa kimajukumu, wana nafasi kubwa ya kushiriki mara kwa mara kwenye maonyesho yake, katika kumbi anazotumbuiza.

Tofauti na sie ambao hivi sasa tunaitwa baba ama babu, ambao kutokana na familia kututaiti, tumejikuta mara nyingi tukibaki kushabikia nyumbani tu, kwenye radio na runinga zetu.

Sasa, kama mabrazamen na masistaduu ndio wanazi wa kwanza wa bendi kama Extra Bongo, basi pamoja na mambo mengine, Choki angehakikisha anakuwa na kikosi chenye wasanii ambao ni vipenzi wa watu hao.

Ninapozungumzia kikosi chenye wasanii ambao ni vipenzi na hao masistaduu na masharobaro, hapa nawagusa zaidi wale ambao rika zao zinashabihiana nao.

Tija ya kuwa na wasanii vipenzi wa masharobaro tunaona inavyozibeba bendi kama vile ‘Twanga Pepeta’, ‘FM Academia’, ‘Akudo Impact’ pamoja na ile iliyoibuka kwa kishindo na kukubalika vilivyo hivi sasa, ‘Mapacha Watatu’.

Kwa hali ya kibiashara katika soko la muziki ilivyo hivi sasa kwenye bendi za dansi la kizazi kipya kama Extra Bongo, ukimchukua msanii kutokana na kipaji chake tu, bado hujafanya kitu.

Kwa hoja hii, naomba isiwe nimejenga chuki kati yangu na wanamuziki ambao si masharobaro, japokuwa ukweli ndio huo na Choki kama Kiongozi wa Extra Bongo anatakiwa achekeche akili yake ipasavyo.

Kwakuwa, katika ‘line up’ ya uimbaji katika kundi lako unaweza kuwa na mkongwe mmoja ama wawili tu, kisha wengine waliosalia wote wakawa ni ‘watoto wadogo’.

Kwa leo naomba niishie hapo, ila kama ilivyo kawaida, mwisho wa mada ya wiki hii ndio mwanzo wa mada ya wiki ijayo, nawatakia Sabasaba njema, tukutane Ijumaa ijayo.

Habari na Abdallah Mensah

Login to post comments

MSANII WA WIKI

Loveness

MUIGIZAJI na Mtayarishaji wa Filamu Tanzania Loveness Watson Nyota yake kwa sasa inatingisha katika tasnia ya

Soma Zaidi...

VIDEO YA MHARIRI

Off Side

Si mara ya kwanza kutazama filamu za Kanumba, lakini pia ni ukweli kwamba kila filamu anayokuja nayo

Soma Zaidi...

FILAMU ZA BONGO

Mbawa za Dino Zafunguka

MUIGIZAJI na Mtayarishaji wa filamu hapa nchini Tanzania Dennis Sweya (Dino) anatarajia kuanza kurekodi

Soma Zaidi...

WAHAPAHAPA VIDEO

You need Flash player 6+ and JavaScript enabled to view this video.