11 Julai 2011

Mkutano wa "Mastaa" Watumbukia Nyongo

Mkutano wa "Mastaa" Watumbukia Nyongo

AMANI, utulivu na ustaarabu vilionekana kuwa ni misamiati migumu katika mkutano wa mastaa wa maigizo Bongo na kusababisha pachimbike kufuatia kauli za Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba  kutema mbovu kwa mastaa wanaobambwa na skendo za ngono kila kukicha, Ijumaa Wikienda lina a-z.

Sinema hiyo iliyokosa ‘director’, kama wenyewe ‘wanavyosemaga’, ilijiri Ijumaa ya Julai 8, 2011 ndani ya Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, jijini Dar es Salaam ambapo taasisi hiyo ilikuwa ikifanya mkutano wake wa kawaida.

Ilikuwa pale Mwakifwamba alipoyainua Magazeti Pendwa ya Bongo na kupaza sauti yake akisema wasanii wanaojiita mastaa wamekuwa wakipamba kurasa za mbele kutokana na tuhuma za ngono.

DALILI YA HALI YA HEWA KUCHAFUKA
Awali habari za mkutano huo uliowakutanisha wasanii wote tishio wa Dar zilitua kwenye meza ya gazeti hili hivyo kutuma ‘skwadi’ makini kwenda kushuhudia kitakachojiri.

Hali waliyoikuta katika nyuso za baadhi ya wasanii zilionesha kila dalili ya kutibuka kwa mambo baadaye kwani miongoni mwao walionekana kupania kufanya fujo baada ya masikio ya mapaparazi wetu kunasa kauli zao wakipanga mikakati.

“Mimi sioni hata jambo la maana tuliloitiwa hapa zaidi ya kupotezewa  muda, lakini najua baadaye kutakuwa na hali ya kutoelewana,”  alisikika msanii mmoja mwenye jina kubwa hapa chini, anayeingiza sokoni filamu mfulululizo kila mwezi.

USIKIVU, UTULIVU NA HESHIMA ZIRO
Hatimaye muda wa kuanza kikao ulifika, lakini katika hali ya kushangaza, wasanii wengi waliingia mkutanoni kwa kujivuta huku  wengine wakinywa pombe kama hawana akili nzuri.

JB ANYAMAZISHWA
Katika kuonesha kuwa, hali ya hewa haikuwa nzuri, muda mfupi baada ya kikao kuanza, baadhi ya mastaa  walionekana kukosa maadili licha ya umri na kazi zao kuheshimika kwani walikuwa wakizungumza mambo yao tena kwa sauti ya juu kama wapo majumbani mwao.
Baadhi ya watu waliitafsiri hali hiyo kuwa ni upigaji keleke usio na maana uwanjani hapo.

Jacob Stephen ‘JB’, Issa Mussa ‘Cloud’, Aunt Ezekiel  ‘Gwantwa’, Jennifer Kyaka ‘Odama’ na Steven Mangere ‘Steve Nyerere’ waliongoza kwa kupiga kelele hali iliyomfanya Mshereheshaji wa mkutano huo ‘MC’ kumtaja kwa jina  JB akimtaka atulie.
Staa huyo wa Filamu ya Senior Bachelor alionesha kukosa amani akiamini alidhalilishwa kama siyo kuaibishwa.

MAOVU YAANIKWA
Upepo ulianza kugeuka kwa kasi ya kimbunga  baada ya  muigizaji aliyejizolea jina kubwa katika Kipindi cha Bongo Dar es Salaam cha TBC1, Kulwa Kikumba ‘Dude’ kupewa nafasi ya kuzungumza kabla ya kumkaribisha Rais wa TAFF, Mwakifwamba.

Dude alisema kuwa, kwa sasa wasanii wanaharibu maana ya sanaa nchini kwani matendo wanayoyafanya hayaendani kabisa na thamani yao katika jamii.

“Sasa hivi sanaa imekuwa kama choo, yaani mtu haiingii na hodi, machangudoa na watu wahuni wamevamia sanaa ya filamu. Picha nyingi za nusu uchi na ngono vimeshamiri,” alisema Dude.

WOLPER ALIANZISHA
Baada ya Dude, Rais Mwakifwamba akashika ‘maiki’ na kuanza kutoa dukuduku lake akishusha tuhuma kwa wasanii, hasa wa kike, kufumba na kufumbua, Jacqueline Wolper alivamia jukwaa akitaka kumtwanga bosi wake huyo na kuanzisha fujo ya kihistoria iliyotibua shughuli.

Kama siyo Deogratius Shija kumshika, si ajabu kichwa cha habari kwenye gazeti hili kisingekuwa PACHIMBIKA.
Wasanii wengine nao waliporomosha ‘paragrafu’ za matusi zisizochoreka gazetini kwa kuzingatia maadili, pia wapo waliorushiana makonde.

Habari zinapasha kuwa, Wolper alifikia uamuzi wa kumkabili bosi wake huyo baada ya skendo ya wasanii wa kike kujiuza kwa mapedeshee kutajwa.

Ilimlazimu Rais Mwakifwamba kusitisha hotuba yake kwani hakukuwa na maelewano tena eneo hilo, vurugu kila mahali huku JB na Steve Nyerere nao wakitaka kupanda jukwaani kwenda kumrudi ‘laivu’ kiongozi wao huyo na kuzuiwa na Rado.

POLISI WAOKOA JAHAZI
Kuona sasa kitumbua chao kitaingia mchanga kwa ‘kuruhusu’ fujo, Vijana wa Mwema (polisi) walitumia madaraka yao kuokoa mtifuano huo kwa kuwataka wasanii waache jazba na badala yake wafuate utaratibu wa kisheria vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale watakaokwenda kinyume.

KAULI ZA WASANII
Baada ya hali ya hewa kuonekana kutulia, baadhi ya wasanii walianza kukusanyika katika makundi wakitoa kauli juu ya vurugu hizo.

Kanumba: “Nilikuwa natafuta njia ya kujitoa rasmi TAFF, sasa hii imechangia, mambo gani haya tunafanyiana, mbona haki haitendeki, tunadhalilishana.”
Coud: “Ustaarabu gani huu? Mbona mnashindwa kuwa waungwana, mnafikiri ni sifa kutamka maneno ya namna hiyo?”

Hata hivyo, rais huyo na baadhi ya viongozi waliondolewa uwanjani hapo chini ya ulinzi mkali na wasanii wa filamu walifanya kikao cha siri ambacho hawakutaka mtu yeyote kusogea. Lakini kuna habari kwamba, timu ya wasanii ya Bongo Movie imepanga kumpandisha mahakamani Mwakifwamba wakidai amewatukana. Naye amesema yuko tayari.

Habari hii imeandikwa na Brighton Masalu, Gladness Mallya na Shakoor Jongo.  
Wakati huo huo ‘mzimu’ mbaya umemuandama Rais wa TAFF, Simon Mwakifwamba baada ya juzi Jumamosi kunusurika katika ajali mbaya ya gari iliyotokea Tegeta, jijini Dar es Salaam na kuua abiria wanane.

kwa Habari na picha zaidi fuatilia magazeti ya Global Publishers.