Jina la Usajili:  Neno la Siri:    Umesahau neno la siri?   |   Umesahau jina?
18 Julai 2011

Je, Serikali Inaunga Mkono Sanaa Inavyotakiwa?

Je, Serikali Inaunga Mkono Sanaa Inavyotakiwa?

MU hali gani wadau wangu wapendwa wa Kijiwe chenu hiki kitamu cha Burudani, kiwajiacho kila wiki katika siku mwanana na tulivu kama ya leo, yaani Ijumaa.

Sina shaka wengi wenu kama si wote, ni wazima wa afya tele na siha njema wakati huu mnapotaradadi kurasa maridhawa za gazeti hili pendwa la Tanzania Daima, huku mkiwa mnaendelea na majukumu yenu ya kujitafutia riziki.

Suala la serikali kutoitilia mkazo ipasavyo sekta ya sanaa ni kilio cha muda mrefu, ambako viongozi walioko katika idara zenye dhamana wamekuwa mara kwa mara wakitupiwa lawama kubwa ya kuwa wamejisahau na kusahau wajibu wao kwa wasanii.

Kelele nyingi zimeshapigwa na wasanii kuhusiana na viongozi wetu kuonekana kujisahau katika hilo bila kuonekana kwa dalili zozote za viongozi hao (wale wenye dhamana) kuamka, kushituka na kuigeukia fani hiyo ya sanaa yenye mashabiki wengi.

Badala yake viongozi wameendelea kuonekana kujitia kuwajali wasanii katika kipindi cha kampeni pekee, ambako huwakusanya kiholela pamoja na vikundi vyao na kuwatumia katika kuvuta wapiga kura wakiwahadaa kwa vijisenti na fulana zenye picha za wagombea.

Hata hivyo taarifa zilizosambaa hivi sasa katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusiana na viongozi wakuu mbalimbali kuahidi kuhudhuria kwenye tambiko kubwa la kuiombea amani Tanzania, imeanza kuonyesha picha mpya kabisa.

Nasema hivyo kwavile tambiko hilo lililopangwa kufanyika Julai 23, kwenye viwanja vya Temeke Mwembeyanga, jijini Dar es Salaam limeandaliwa na wasanii kutoka vikundi mbalimbali vya Umoja wa Waganga Watafiti wa Magonjwa Sugu kwa Tiba Asili (UMAWATI).

Kwa asilimia kubwa UMAWATI yenyewe inahusika katika kufanikisha uandaaji wa tambiko hilo linalotarajiwa kuanza majira ya saa 2:00 asubuhi na kuendelea hadi saa 9:30 jioni.

Kwa mujibu wa Katibu wa UMAWATI Wilaya Temeke, Juma Kingumba, wasanii wa umoja wao, walikaa na kutafakari kwa kina juu ya mustakabali wa nchi yao, wakaona kuwa kuna haja ya kuiombea amani ili Mwenyezi Mungu aweze kuinusuru.

Wanasema, hii ni kwa sababu Tanzania hivi sasa imeingiliwa na malumbano na mitafaruku mingi ya hapa na pale, hasa katika nyanja za siasa na dini, huku wananchi wake wakiwa katika hatari ya majanga makubwa na ya kutisha kama vile; njaa na maradhi.

Miongoni mwa viongozi waliothibitisha kuhudhuria kwenye tambiko hilo muhimu kwa Watanzania wote ni pamoja na ofisa Utamaduni wa Wilaya ya Temeke, Immanuel Ndumukwa, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Temeke pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Temeke.

Nafarijika sana ninapopata taarifa kama hizi za viongozi wetu kuonyesha kuunga mkono wasanii wetu katika masuala mbalimbali ya kijamii, kwa sababu hiyo inawafanya wasanii hao kuona fahari ya wao kuchagua kazi ya sanaa.

Hawa wa Temeke wameonyesha njia, wito wangu ni kuwa wajitokeze viongozi wengine wengi tu kutoka kwenye ngazi tofauti za serikali, kuanzia zile za mitaa, vijiji na vitongoji hadi Serikali Kuu katika kuwaunga mkono wasanii wetu.

Hii itasaidia kusafisha ‘jina baya’ lililokwisha kujengeka kwa viongozi wetu, la viongozi kutowathamini ipasavyo wasanii katika masuala mbalimbali ya kijamii wakikaa na kungoja kuwaburudisha katika kampeni zao za siasa kwa ujira kiduchu.

Isitoshe sisi sote tunafahamu kuwa, serikali ndio kila kitu hapa nchini na katika nchi nyingine yoyote, hivyo hata katika sanaa tunaamini ndiyo pekee inayoweza kufanya maisha bora kwa kila msanii.

Msiwatupe wasanii wetu jamani, onyesheni kuwaunga mkono katika masuala mazuri mbalimbali wanayofanya kwa nia njema, kwa manufaa ya jamii nzima ya Tanzania kwani bila hivyo hatuwezi katu kuyafika maendeleo ya kweli.

Kwa leo naishia hapa, ila kama kawaida mwisho wa mada ya Ijumaa hii ndiyo mwanzo wa mada ya juma lijalo. Nawatakia wikiendi njema na tukutane wiki ijayo panapo majaliwa ya Mwenyezi Mungu. Amin.

na Abdallah Menssah

Login to post comments

MSANII WA WIKI

Loveness

MUIGIZAJI na Mtayarishaji wa Filamu Tanzania Loveness Watson Nyota yake kwa sasa inatingisha katika tasnia ya

Soma Zaidi...

VIDEO YA MHARIRI

Off Side

Si mara ya kwanza kutazama filamu za Kanumba, lakini pia ni ukweli kwamba kila filamu anayokuja nayo

Soma Zaidi...

FILAMU ZA BONGO

Mbawa za Dino Zafunguka

MUIGIZAJI na Mtayarishaji wa filamu hapa nchini Tanzania Dennis Sweya (Dino) anatarajia kuanza kurekodi

Soma Zaidi...

WAHAPAHAPA VIDEO

You need Flash player 6+ and JavaScript enabled to view this video.