22 Julai 2011

Fiesta, Kunani Paleeee?

Fiesta, Kunani Paleeee?

MSIMU wa matamasha (Fiesta) ambao umebatizwa jina la Msimu wa Dhahabu umekuwa ukiendelea kutoka mkoa huu hadi mwingine.

Msimu huo huwakusanya vijana wengi katika sehemu moja kwa lengo la kubadilishana mawazo huku wakiburudika.

Burudani zinazotolewa katika Msimu wa Dhahabu ni pamoja na wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya Bongo Fleva na baadhi ya vinywaji.

Wanamuziki ambao wamekuwa wakitoa buradani hiyo ni kama vile Prof Jay na Ali Kiba ambao wameingizwa katika shoo itakayofanyika Jumapili ijayo.

Msimu huo kwa kweli umekuwa ukivutia hisia za vijana kwani wamekuwa wakipata nafasi ya kukutana na kufahamiana ama baada ya kupoteana kwa muda mrefu kutokana na majukumu mbalimbali ya kujitafutia maisha.

Hivyo baadhi yao wamekuwa wakitumia muda huo kupeana elimu mbalimbali hususan zile za kujiletea maendaleo katika maisha yao ya kila siku.

Shoo hizo ambazo zimeanza tangu Juni, zimekuwa za mafanikio kwa kiasi fulani lakini hata hivyo katika mafanikio yaliyokusudiwa na waandaaji hata hivyo bado matatizo hayakosekani.

Kama inavyofahamika kuwa unapokusanya makundi ya vijana na kuwaweka sehemu moja ni lazima kutajitokeza changamoto mbalimbali.

Pamoja na waandaaji kuwa na lengo zuri tu la kutoa burudani kwa vijana pamoja na watu wengine wa rika zingine, kumekuwa kukiripotiwa kuwa kuna baadhi ya vijana wasio wastaarabu hufika katika shoo hizo kwa malengo tofauti.

Malengo yao hayo yamekuwa yakienda kinyume tofauti na kile kilichokusudiwa na waandaaji.

Vijana hao wamekuwa wakijiingiza katika vitendo vya kuutia dosari musimu huo kwa kufanya vurugu ambazo kiukweli zinaharibu kabisa burudani hizo.

Na hii naweza kusema kuwa imekuwa ni kawaida kila yanapofanyika matamasha kama hayo kujitokeza matukio mabaya ambayo yanaharibu maana na kufanya ionekane kuwa matamasha hayo hayana maana.

Hali hiyo ya vurugu ni kama zile zilizotokea hivi karibuni kule mkoani Arusha kwa baadhi ya washiriki kufanyiana vurugu hadi kufikia hatua ya kuchomana visu katika ugomvi ambao unadaiwa ulitokana na visa mbalimbali.

Visa vikubwa vinavyotajwa kuwa chanzo cha magomvi yao ni kugombea wanawake ama kulewa kupita kiasi ambapo wengine hujiingiza katika ukabaji wa kupora mali za washiriki wenzao.

Inasemekana hali katika tamasha hilo la Arusha ilikuwa ya vurugu sana ambapo wengi wa washiriki wakiwa wamepoteza mali zao, kubakwa na kujeruhiana.

Sidhani kama lengo haswa la matamasha haya ni hayo madudu kwani kama hali ikiendelea hivyo basi itafikia kipindi maonyesho hayo yatapigwa marufuku.

Haipendezi hali kama hiyo kujirudia rudia kila wakati na sasa baadhi ya wazazi wameanza kuyapinga matamasha hayo.

Wamekuwa wakidai matamasha hayo hayana manufaa wala hayawasaidii chochote vijana wao zaidi ya kuwaingiza katika matendo mabaya kama vile vitendo vya ngono zembe ambayo ni hatari sana haswa katika kipindi kama hiki cha ukimwi.

Adha, baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwatupia lawama waandaaji wa matamasha hayo kuwa wamekuwa wanufaika katika biashara zao huku wakiwaachia watoto wao hasara.

Katika wazazi hao wapo wanaotaka kujua hivi kuna faida gani ya kuwa na matamasha kama hayo ama wandaaji na washiriki wanapata faida gani?

Mtazamo wangu katika hili naweza kusema kwa kinywa kipana kabisa kuwa kuna mapungufu kutoka kwa waandaaji kutokana na mipango mibovu ya kiusalama.

Nasema hivyo, kutokana uzoefu wa Fiesta nyingi ambazo zimewahi kufanyika ambapo zote zimekumbwa na matatizo kama hayo.

Kutokana na matatizo kama hayo nilidhani waandaaji wangepata somo la kuja na mikakati mipya ya kuyadhibiti magenge ya wahuni wanaokwenda kwenye matamasha hayo kwa lengo la kufanya unyama.

Sitaki kwenda mbali zaidi na kutoa dosari nyingi ambazo hata Mwanza yalitokea magenge hayo, labda cha msingi kwa kuwa matamasha hayo yanapendwa na vijana ni bora waandaaji wakajipanga vizuri na kuyaboresha na yakawavutia wengi zaidi.

Na uboreshaji wa matamasha hayo ni kuimarisha ulinzi pia kuwe na malengo ambayo ni ya maana na kimaendeleo kuliko ya sasa ambayo ni kama kuumizana, kujifunza ngono na ulevi kwa baadhi ya vijana.

Aidha, waandaaji wanatakiwa kuwa karibu na vyombo vya usalama kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na kulinda mali za washiriki na wengine katika maeneo yanapofanyika matamasha hayo.

Natarajia mfano mzuri utaanzia katika tamasha litakalofanyika hivi karibuni mkoani Tanga ambapo litarudisha imani kwa wale wote waliokuwa wakidhani asili ya matamasha hayo ni vurugu tu na si kingine.

Na Shehe Semtawa