Jina la Usajili:  Neno la Siri:    Umesahau neno la siri?   |   Umesahau jina?
25 Julai 2011

Harambee Tiba ya Gurumo Yafana

Harambee Tiba ya Gurumo Yafana

ONYESHO maalum lililoandaliwa na Mkurugenzi wa African Stars ‘Twanga Pepeta’ Asha Baraka, la kuchangisha fedha kwa ajili ya kumpatia kiongozi wa Msondo Ngoma, Muhidin Gurumo, aliyelazimika kujistaafisha muziki kutokana na kuumwa, lilifana.

Onyesho hilo lililofanyika juzi usiku kwenye ukumbi wa Mango Garden, ulioko Kinondoni jijini Dar es Salaam, lilipokelewa vema na wapenzi na wadau wa muziki kwa ujumla ambao walichangia fedha za kutunisha mfuko wa kumsaidia mwanamuziki huyo.

Akizungumza katika uzinduzi wa harambee hiyo, mgeni rasmi Naibu Meya wa Kinondoni, Songoro Mnyonge, alianza kwa kumshukuru na kumpongeza mratibu wa tamasha hilo Asha Baraka na bendi nzima ya Twanga Pepeta kwa kuona thamani ya mwanamuziki huyo.

“Kabla ya yote nichukue fursa hii kumshukuru na kumpongeza Asha Baraka na bendi nzima ya Twanga Pepeta kwa uamuzi wao wa kuandaa onyesho maalum la kumchangia mzee wetu, Muhidin Gurumo, ambaye amestaafu muziki kwa sababu ya maradhi,” alisema Songoro na kuongeza:
“Wakati nikiongea naye mzee Gurumo ameniambia kuwa alianza muziki mwishoni mwa 1950 na kufikia mwaka 1961 wakati nchi yetu ikipata Uhuru tayari alikuwa mwimbaji, huu ni muda mrefu kweli, leo tunapozungumza ana miaka 71 na alikuwa bado anaimba kama sio maradhi,” alisema na kushangiliwa.

Alisema wanamuziki hawana malipo ya uzeeni, basi kitendo kilichofanywa na Asha kinastahili kupongezwa na kuigwa na wadau wa muziki na wana jamii kwa ujumla kwa sababu fedha zitakazopatikana katika harambee hiyo zitamsaidia sana mlengwa katika maisha yake mapya nje ya muziki.

Katika harambee hiyo wadau waliweza kuchangia zaidi ya shilingi milioni 2 taslimu, mbali ya fedha zilizopatikana kutokana na viingilio vya waliohudhuria ambazo kwa mujibu wa Asha atakabidhiwa Gurumo ili ziweze kumsaidia.

Mbali ya Twanga Pepeta na Msondo Ngoma kupagawisha walipotumbuiza kwa nyakati tofauti, lakini mashabiki na wadau waliohudhuria onyesho hilo, walipagawa zaidi pale mzee Gurumo mwenyewe alipopanda jukwaani kuwasalimia na kuamua kuimba wimbo mmoja.

Kila aliyemsikia mzee Gurumo akikumbushia enzi zake kwa kuimba wimbo ‘Piga ua Talaka Utatoa’, alinyanyuka na kujisachi chochote alichonacho na kwenda kumtunza, kutokana na jinsi alivyoimba na kuacha minong’ono ukumbini kila mmoja akisema lake.

Kipande cha Gurumo katika wimbo huo kilichowapagawisha watu ni kile kisemacho “Jitihada zake zote zimegonga ukuta, kwa kutangazia ubaya kwa majirani zakee, mara hivi mara vile kutengena kwenu kusiwe chanzo cha uhasama.”
Naye Asha Baraka alisema kuwa huo ni mwanzo tu wa kumsaidia mzee Gurumo, kwani kwa sasa wana mpango wa kuandaa onyesho lingine kubwa litakaloshirikisha bendi nyingi zaidi wakiamini pato litakalopatikana litakuwa kubwa la kumuwezesha kuendesha maisha bila wasiwasi.

Alisema pia wataangalia kama itawezekana waweze kufanya maonyesho ya aina hiyo pia mikoani ambako wanaamini Gurumo anao wapenzi wengi na ambao watakuwa tayari kumchangia chochote walichonacho.

na Ruhazi Ruhazi

Login to post comments

MSANII WA WIKI

Loveness

MUIGIZAJI na Mtayarishaji wa Filamu Tanzania Loveness Watson Nyota yake kwa sasa inatingisha katika tasnia ya

Soma Zaidi...

VIDEO YA MHARIRI

Off Side

Si mara ya kwanza kutazama filamu za Kanumba, lakini pia ni ukweli kwamba kila filamu anayokuja nayo

Soma Zaidi...

FILAMU ZA BONGO

Mbawa za Dino Zafunguka

MUIGIZAJI na Mtayarishaji wa filamu hapa nchini Tanzania Dennis Sweya (Dino) anatarajia kuanza kurekodi

Soma Zaidi...

WAHAPAHAPA VIDEO

You need Flash player 6+ and JavaScript enabled to view this video.