28 Julai 2011

Irene Uwoya Aitwa Ikulu

Irene Uwoya Aitwa Ikulu

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunzinza hivi karibuni alimtumia ujumbe mwigizaji maarufu wa filamu Bongo, Irene Uwoya (pichani) akimtaka aende Ikulu kwake kwa ajili ya mazungumzo, Amani lina habari kamili.

Akizungumza na mwandishi wetu Julai 25, mwaka huu, Uwoya alisema Rais Nkurunzinza alimuita baada ya kusikia kuwa yupo nchini kwake na amevuta hisia za wengi.

“Nilipokwenda Burundi kwa ziara ya kisanii Rais Nkurunzinza alipata taarifa, akaambiwa nimeitingisha sana nchi yake. Kutokana na taarifa hizo alitaka kuniona, akanitumia gari na ulinzi wa polisi ili waje kunichukua.

“Kwa kuwa sikuwa na muda mrefu wa kukaa Burundi kufuatia kutakiwa kurudi haraka Cyprus kwa mume wangu, ilibidi nikatae,” alisema Uwoya.

Akaongeza kuwa, licha ya kipindi hicho kushindwa kuonana na rais huyo, bado amekuwa akiendelea kumsihi atafute siku amtembelee hivyo ameamua kutimiza hilo atakapoacha kumnyonyesha mwanaye.

“Sikuwahi kuwaza kama kuna siku ningeweza kwenda nchi yoyote na kukusanya umati mkubwa wa watu kiasi kile, pia sikuwahi kuota kama siku moja ningeweza kuwa staa wa kuombwa kukutana na kiongozi maarufu wa nchi yoyote kama ilivyotokea kwa Rais wa Burundi.

“Kwa sasa bado najipanga, nitaenda kuonana naye pindi mwanangu atakapoacha kunyonya kwani ni bahati kwangu kukutana na kiongozi huyo kupitia kazi zangu za kisanii,” alisema Uwoya.