Jina la Usajili:  Neno la Siri:    Umesahau neno la siri?   |   Umesahau jina?
25 Machi 2011

Tuamke, Wakati Ukuta...

Tuamke, Wakati Ukuta...

Washkaji mambo vipi? Ni matumaini yangu makubwa kwamba hali si mbaya na mnaendelea vyema na pilikapilika za kupambana na makali ya maisha au siyo?

Kama hivyo ndivyo, basi mtu wangu acha leo nizungumzie kuhusu wale wasanii wa muziki wa Bongo-Flava, ngoma ambazo zilikamua ile mbaya

na hadi sasa wanaendelea kutesa kwenye medani ya muziki huo.

Kama hiyo haitoshi, watu wangu napenda kuwauliza vipi mbona ‘game’ kama linawaweka katika makundi, yaani kuna waasisi, waliotesa, waliopotea na chipukizi, vipi mambo yanakuwa hivi jamani?

Hivi huwa mnapata muda wa kubadilishana mawazo na kunyooshana pale mmoja anapopinda, au ndiyo shaghalabaghala tu?

Watu wangu amkeni, hebu waangalieni wasanii wenzenu wanaocheza michezo ya kuigiza, wameingia mtaani juzi kati tu hapa lakini mambo yao ni mazuri na uzuri ninaouzungumzia mimi hapa ni umoja na mshikamano walionao.

Katika hili nawapa pongezi nyingi wasanii wa tasnia ya filamu nchini, endeeleeni hivyo hivyo, ipo siku nanyi mtakuwa juu kama walivyo wenzenu wa NollyWood, Holly Wood na Bollywood.

Turudi kwa wasanii wetu wa Bongo-Flava, hasa wale wenye majina makubwa kuwa tayari kukutana, ili kuleta chachu kwa wasanii chipukizi ili nanyi muwe kitu kimoja. Litakuwa jambo zuri na lenye kuwaletea ufanisi katika kazi zenu, au sio jamani?

Nina imani kubwa kwamba endapo wale wasanii wenye majina wakiamua, Inshaallah, watafanikiwa. Kwani wataleta chachu kwa wasanii chipukizi hasa wale wenye njozi za kuwa kama Ambwenye Yessaya ‘AY’, Khamisi Mwinjuma ‘Mwana FA’ na wengineo wa kaliba hiyo.

Kama hiyo haitoshi, nina matumaini makubwa kwamba endapo nanyi mtaunda umoja wenu, mtaweza kusaidiana kwa namna moja au nyingine ikiwa ni pamoja na kupeana mawazo. Hiyo inatosha kuliko jinsi mlivyo sasa kwani kila mtu na lwake, tena nakumbuka kuna wakati BASATA ilijaribu kuwasaidia kuunda chama chenu na kuwapa hadi ofisi.

Nakumbuka kulikuwa na chama cha wafokaji (Tanzania Rappers Association), kilichofuatiwa na chama cha muziki wa kizazi kipya (TUMA), Tanzania Urban Music Association.

Tena hiki kilifikia kuchagua viongozi kama vile Basil Kashumba ‘K-Basil’ (Mwenyekiti) na Stara Thomas (Katibu), ambacho nimepata fununu kuwa kimeanza upya mchakato wa kujifufua ili kijumuishwe katika mpango wa mashirikisho ya vyama vya wasanii kupitia uchagizaji na msaada wa BASATA.

Wakati umefika sasa hata kama msanii atasimamia kazi zake, lakini umoja ni muhimu na kitu chenye manufaa kwenu, hivyo lifikirieni suala hili kwa makini.

Pia nadhani kwa kupitia umoja huu mtaweza kujitangaza nje ya mipaka ya nchi, huku hata watu wanaohitaji kuwapata wasanii na kuhitaji kuwatumia katika kazi zao mbalimbali, watajua wapi pa kupata taarifa zote muhimu.

Hebu jifunzeni kwa wenzenu wa filamu ambao wamefanikiwa kwa muda mfupi licha ya kuwa na upungufu fulani fulani, kwa kuwa lazima pawe na pa kuanzia. Hivyo acha tuwape sifa zao kwa kufanikiwa kurusha filamu zao kwenye kituo cha ‘Africa Magic’, ambapo hapo awali filamu za NollyWood ndizo ziliteka ulingo huo.

Ila kwa sasa mambo si mabaya, kwani Mtanzania popote alipo sasa anatambulika, kuwa hatuko nyuma katika masuala ya kuigiza, licha ya kuwa mwanzo mgumu.

Vivo hivyo nanyi wa Bongo-Flava unganeni na mjitume ili sisi wabongo tuliopo nyuma yenu tuone mnatamba katika vituo mbalimbali vya televisheni barani Afrika, kama zinavyotamba ngoma nyingine za wasanii wa Kiafrika.

Ikumbukwe kwamba endapo nyote mtakuwa na sauti moja itawasaidia katika mambo mengi, jambo ambalo hadi hivi sasa linaonekana wadau bado hawajaling’amua.

Kama hiyo haitoshi, wasanii hao hao ambao ndio wahusika wamekuwa wakirudi nyuma hata pale wanaposhikwa mkono, kwani nimeweza kuhudhuria makongamano mbalimbali huku wengi wao wakishindwa kuitikia wito huku wahudhuriaji wakiwa wachache, jambo linalowakatisha tamaa waandaaji na wasanii waojaribu kuhudhuria.

Hivi karibuni Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) likishirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni (CAJA), limeanzisha midahalo ya kila siku ya Jumatatu kujadili matatizo mbalimbali ya wasanii.

Mshikadau mmoja kutoka mkoani Morogoro ameupongeza utaratibu huo, huku akisema kwamba BASATA wanashiriki kusimamia na kuwasaidia wasanii ili wafanikiwe kwa kupata haki zao na hatimae watimize malengo yao kimaisha.

Lakini wasanii wengi ambao maskani yao ni hapa jijini wamekuwa wakiingia mitini, hawahudhurii midahalo hiyo, sasa watasaidiwa vipi watu kama hawa?

Mdau huyo ambaye anaongoza kwa kusema kwamba licha ya yeye kuishi mji kasoro bahari - Morogoro na majukumu kibao aliyonayo, lakini anajitahidi kuhudhuria licha ya gharama za nauli kutokana na umbali uliopo.

Lakini amewashangaa hawa wanaoishi kwa nauli za daladala kama si teksi au kutia mafuta kwenye magari yao, wanapoitwa hawaonekani!

Vunjeni roho hii ya utengano miongoni mwenu, acheni ubaguzi na hulka ya kila mmoja kujiona yeye ana thamani zaidi ya mwingine, mtafanikiwa. Au naweza kusema kwamba huu ni woga?

Kwani hata Waswahili husema ‘kaburi chakavu la shujaa ni bora kuliko nyumba angavu ya mtu mwoga,’ hivyo basi msipojiamsha kwenye lindi hili la usingizi mtalala daima na kuendelea kumsaka mchawi huku wenzenu wakiendelea kuchanja mbuga kwa kupata mafanikio.

Kumbukeni kwamba muziki ni ajira kama zilivyo ajira nyingine, ambayo mtailinda kwa katiba nzuri itakayokuwa dira kwenu na kizazi kijacho.

Habari na DHW

Login to post comments

MSANII WA WIKI

Loveness

MUIGIZAJI na Mtayarishaji wa Filamu Tanzania Loveness Watson Nyota yake kwa sasa inatingisha katika tasnia ya

Soma Zaidi...

VIDEO YA MHARIRI

Off Side

Si mara ya kwanza kutazama filamu za Kanumba, lakini pia ni ukweli kwamba kila filamu anayokuja nayo

Soma Zaidi...

FILAMU ZA BONGO

Mbawa za Dino Zafunguka

MUIGIZAJI na Mtayarishaji wa filamu hapa nchini Tanzania Dennis Sweya (Dino) anatarajia kuanza kurekodi

Soma Zaidi...

WAHAPAHAPA VIDEO

You need Flash player 6+ and JavaScript enabled to view this video.