Jina la Usajili:  Neno la Siri:    Umesahau neno la siri?   |   Umesahau jina?
29 Machi 2011

Dede Azungumza

dede

MACHI 15, mwaka huu, msanii na mwimbaji mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Shaaban Hamad, maarufu kwa jina la ‘Dede’, aliihama bendi ya Sikinde Ngoma ya Ukae, ambayo aliitumikia kwa miaka 20 na kurudi katika bendi ya Msondo Ngoma.

Ilikuwa ni vigumu kwa wanamuziki wenzake wa bendi ya Sikinde na mashabiki kukubali na kuamini kwamba Dede, ameamua kurudi katika bendi yake ya zamani ya Msondo Ngoma, ambayo aliitumikia kwa zaidi ya miaka 10.

Lakini hali imekuwa ndiyo hiyo. Kutokana na kauli yake mwenyewe Dede kwa wanamuziki wenzake wa bendi ya muziki, mashabiki na hata kwa vyombo vya habari amesema kwamba ameamua kurudi nyumbani.

“Nataka niwatoe hofu ndugu zangu wa Sikinde, mashabiki na hata waandishi wa habari kwamba nimeamua kurudi nyumbani Msondo, kwani nyumbani ni nyumbani, Sikinde hakuna tatizo lolote bali nimeamua tu kurudi,” anasema Dede na kuongeza:

“Kurudi kwangu Sikinde nadhani ni mipango ya Mungu, hivyo nawaomba wanamuziki wenzangu wa Sikinde, bendi zingine na wapenzi wangu, waendelee kunipa ushirikiano, kwani huu ni uamuzi wangu,” anasema Dede.

Anajifananisha na jembe Ulaya kwamba, yeye kama mwanamuziki mkongwe wa dansi, yuko tayari kupokea mawazo ya wapenzi na kushirikiana na mwanamuziki ambaye atahitaji msaada wake wakati wowote na mahali popote yuko tayari.

Anasema tangu mwaka 2008 alifanya uamuzi wa kurudi Msondo Ngoma lakini, uamuzi wake ulikuwa ukikatizwakatizwa na wanamuziki wenzake wa Sikinde, King Enock na Bitchuka kwamba aendelee.

Dede anasema akiwa Sikinde kama mwimbaji na hapo hapo mweka hazina wa bendi hiyo, amefanikiwa kukua kimuziki pamoja na kupata umaarufu kutokana na bendi hiyo kuwa kubwa na kuwa na wapenzi wengi.

Anasema kamwe hawezi kuisema vibaya bendi hiyo kutokana na umahiri wa wanamuziki wake ambao wanaipenda kazi yao na kuifanya pasipo manung’uniko ya aina yoyote ile wanapokuwa katika mazoezi na hata maonyesho.

“Sitaki kusema uongo, maisha yangu ya miaka 20 nikiwa sikinde sijawahi kuona mwanamuziki yeyote anafanya vurugu ama kudai masilahi zaidi, wote kwa pamoja tuliridhika kwa kile tulichokipata kutokana na shoo tunazozifanya,” anasema.

Akiongeza kutoa sifa kwa bendi hiyo ya Sikinde, anasema kuwa imekamilika kila upande, kuanzia ngazi ya chini hadi juu chini yake, Hamid Jefu na kwamba hakuna dosari zozote na hata katika mapato.

Anasema kwa kuwa wanamuziki wa Sikinde wanayo nafasi sawa katika uimbaji, anao uhakika kuwa kuondoka kwake hakutaweka pengo lolote, hivyo anawataka wakamilishe malengo waliyojiwekea na hata kuzidisha.

Dede anasema ukongwe na umaarufu alionao umetokana na nyota yake kung’ara mwaka 1972, baada ya kutoka shuleni na kuanza kuimbia bendi ya Vijana wa Chama cha Tanu ‘Youth five’ huko Biharamulo, mkoani Kagera.

Mwaka 1972 alihamia Bukoba mjini na kujiunga na bendi ya Polisi Jazz hadi mwaka 1977 alipoihama na kujiunga na bendi ya Aluta Continua ya hukohuko Bukoba kabla ya kwenda Mirambo, Tabora kujiunga na bendi ya Wanasomasoma ‘Tabora Jazz’.

Mwaka 1979 hadi 1989 alijiunga na bendi za Msondo na Mlimami Park, ambazo zote kwa pamoja aliweza kuzitumikia ipasavyo hadi mwanzoni mwa mwaka 1990.

Anasema aliamua kupumzika kazi za muziki kwa mwaka mmoja (1990) kutokana na miaka hiyo kuwapo kwa ushabiki mkubwa wa mpira pindi walipocheza mahasimu wawili - Simba na Yanga.

Dede anasema katika kipindi hicho akiwa nje ya fani ya muziki, aliweza kufanya kazi ya kutengeneza na kuendesha magari kutokana na kuijua vema fani hiyo.

Anasema akiwa katika shughuli hizo huku akiwa shabiki mkubwa wa timu mojawapo ya mahasimu hao, aliitwa na Muhidin Gurumo pia aliwahi kualikwa katika bendi ya Bima na kuwa mgeni rasmi katika moja ya maonyesho na hapo hapo akaamua kurudi katika fani ya muziki tena.

“Niliamua kujiunga na kufanya kazi na bendi ya Sikinde Ngoma ya Ukae. Mwaka 2008 nilianza kufikiria kurudi nyumbani, wenzangu walinisihi nibaki, lakini naona nirudi, kwani nyumbani ni nyumbani tu,” anasema Dede.

Akizungumza na mwandishi wa makala hii, kiongozi wa bendi ya Msondo Ngoma, Said Mabera, anasema: “Kurudi kwa Dede Msondo kutaipandisha kiwango bendi hiyo, kutokana na umahiri wa mwimbaji huyo mkongwe.”

Login to post comments

MSANII WA WIKI

Loveness

MUIGIZAJI na Mtayarishaji wa Filamu Tanzania Loveness Watson Nyota yake kwa sasa inatingisha katika tasnia ya

Soma Zaidi...

VIDEO YA MHARIRI

Off Side

Si mara ya kwanza kutazama filamu za Kanumba, lakini pia ni ukweli kwamba kila filamu anayokuja nayo

Soma Zaidi...

FILAMU ZA BONGO

Mbawa za Dino Zafunguka

MUIGIZAJI na Mtayarishaji wa filamu hapa nchini Tanzania Dennis Sweya (Dino) anatarajia kuanza kurekodi

Soma Zaidi...

WAHAPAHAPA VIDEO

You need Flash player 6+ and JavaScript enabled to view this video.