Jina la Usajili:  Neno la Siri:    Umesahau neno la siri?   |   Umesahau jina?
29 Machi 2011

Bongo Celebrity Yateta na 20%

20%

Zoezi la utoaji wa Kili Tanzania Music Awards lilipomalizika hapo juzi pale Diamond Jubilee Hall jijini Dar-es-salaam,jina moja lilibakia katika vinywa na bongo za mashabiki wa muziki na wote waliofuatilia tuzo hizo.Jina hilo sio lingine bali la Abbas Hamisi au maarufu kama kwa jina la kisanii la 20%.

Kijana huyo mzaliwa wa mkoa wa Pwani ambaye unaweza kusema bado ni msanii asiyejulikana sana hususani nje ya mipaka ya Tanzania,aliibuka “Mfalme” kwa kutwaa jumla ya tuzo 5 miongoni mwa vipengele 7 alivyokuwa ameteuliwa katika kuwania tuzo hizo. Kwa ujumla 20% aliibuka mshindi kama Male Artist of The Year(Msanii Bora wa Kiume), Best Male Singer(Mwimbaji Bora wa Kiume), Best Song Writer of The Year(Mwandishi Bora wa Nyimbo wa Mwaka) na huku kibao chake cha Tamaa Mbaya kikiibuka mshindi katika kipengele cha Best
Song of The Year(Wimbo Bora wa Mwaka) na Ya Nini Malumbano kikiibuka mshindi katika Best Afro Pop Song(Wimbo Bora wa Afro Pop).

Kwa bahati mbaya, 20% hakuwepo ukumbini kupokea tuzo zake na badala yake producer wake John Shariza “Man Water” kutoka Combinations Sounds ndiye alikuwa na kazi ya ziada ya kuzibeba tuzo 5 za 20%.
Kwanini yeye mwenyewe hakuwepo pale Diamond Jubilee Hall kupokea tuzo zile?Ni jinsi gani ameupokea ushindi huo? Kwanini anajiita 20%? Baada ya tuzo hizo,nini kinafuata katika maisha yake au kazi zake? Ili kupata majibu ya maswali hayo na mengineyo,BC ilimtafuta 20% .Fuatilia mahojiano yafuatayo;

BC: Mambo vipi 20%?

20%: Ee bwana mimi Mungu ananisaidia,sijui wewe brother.

BC: Yuko nasi pia.Kwanza hongera sana kwa ushindi wako wa juzi.Awards tano kwa mkupuo sio mchezo.Hongera sana

20%: Ni kweli kabisa Bro.Hata mimi namshukuru sana Mungu kwa kuniwezesha kuibuka mshindi namna ile.

BC: Labda swali la kwanza ambalo watu wengi wangependa kujua ni ilikuwaje ukakosa kuhudhuria shughuli ya utoaji wa tuzo zile? Nini kilitokea?

20%: Kwa kweli hata mimi mwenyewe nilisikitika kutokuwepo pale.Ilitokea tu kwa bahati mbaya nilikuwa na show nyingine ya kijamii mjini Tabora ambayo nilishaifanyia booking muda mrefu sana uliopita.Kwa hiyo ilinibidi kwenda kule kwa sababu kama unavyojua katika show huwezi kutuma mwakilishi kama ambavyo unaweza kufanya au nilivyofanya katika tuzo za Kili.

BC: Hilo linaeleweka na naamini mashabiki wako watakuwa watakuelewa.Sasa zile taarifa kwamba umeshinda ulizipataje na ulizipokea namna gani?

20%: Taarifa za ushindi ule nilizipata kupitia luninga kwa sababu nilikuwa sehemu fulani nikifuatilia kila kitu kupitia ITV kabla ya kwenda kwenye show yetu.Pale nilipokuwa nilifuatilia mpaka niliposhinda award ya nne ndio jamaa wakanifuata kwamba sasa twende kwenye show.Taarifa za award ya tano nilizipata nikiwa tayari nipo kwenye show pale Uwanjani Tabora.
Kwa kweli nilifurahi sana sana sana kupata ushindi ule.

BC: Sasa kuna baadhi ya mashabiki wamekuwa wakijiuliza huyu 20% ni nani?Hawa ni wale ambao walikuwa hawajawahi kufuatilia kwa karibu miziki yako au kazi zako za kiusanii.Labda kwa faida ya mashabiki hao ambao hawakufahamu,wale ambao juzi ndio ilikuwa mara ya kwanza kusikia jina lako…jina lako kamili ni nani na kwanini uliamua kujiita 20%?

20%: Jina langu kamili ni Abbas Hamis. Ni mzaliwa wa Mkoa wa Pwani.Ni mtoto wa pili katika watoto wa kiume wa mzee wangu.
Hili jina la 20% nililipata kutokana tu na jinsi mimi mwenyewe nilivyokuwa najiona.Hata wewe mwenyewe kama utabahatika kusimama na mimi,utajua mimi kweli ni 20% kutokana na kimo na maumbile.
Halafu pili mimi najitambua kama 20% kimatendo kwa sababu tofauti na labda watu wengine mashuhuri au matajiri duniani ambao wanaishi kwa kutegemea utajiri waliorithi au akili nyingi walizopewa na Mungu na mambo kama hayo,mimi natumia akili yangu ndogo kuishi na kufanya mambo yangu kitu ambacho kitu ambacho mimi nakiona ni 20% yaani kulinganisha akili yangu na labda za wale manabii wa hapo zamani.

BC: Sasa nikisikiliza nyimbo zako tangu umeanza,nyimbo kama vile Maisha ya Bongo akaelezea jinsi ya watu wanavyochomwa moto, vijana hawana muelekeo n.k.; yaani suluba zinazowakuta vijana wa Uswazi n.k.ulikuwa kwenye mahadhi ya Hip Hop zaidi kwa (mtazamo wangu). Ingawa bado unazungumzia mambo yale yale (Heko kwa hilo), kwanini amebadilisha style kidogo? Au alikuwa anajitambulisha tu?

20%: Ni kweli kwamba kuna mabadiliko kidogo hususani katika midundo nk.Kwa ujumla mimi natumia style mbalimbali.Utaona kwa mfano wimbo kama Maisha ya Bongo upo kwenye mtindo wa Reggae zaidi wakati wimbo kama Money Money uko katika mahadhi ya Pop zaidi.
Na mimi mwenyewe jambo moja ambalo labda watu wengi hawajui ni kwamba ni mtunzi mzuri wa nyimbo za mitindo tofauti tofauti kama vile Reggae,Hip Hop,Zouk nk.Kwa hiyo kinachotokea hivi sasa ni kwamba naziandika nyimbo zangu katika fikra za ki-hip hop na kisha kuziimba katika mahadhi tofauti tofauti.

BC: Hivi karibuni kumekuwa na hoja kwamba mwelekeo wa Bongo Fleva kwa ujumla umekuwa kama haueleweki, lakini inaonekana yeye sasa hivi (hata kabla ya kuchukua tuzo) ndio “icon” ya muziki wa Tanzania. Wengine wanaufananisha uwepo wako katika muziki wa kizazi kipya na kama vile alivyo Chameleon kule Uganda. Je, unachukuliaje maoni kama hayo? Je ni jukumu ambalo uko tayari kulibeba au inakuwaje?

20%: Nianze kwa kusema nashukuru kusikia sifa kama hizo kwa sababu najua Chameleon ni msanii anayeheshimika vyema kule kwao. Lakini kiukweli mimi katika maisha yangu nilivyo ni kwamba sipendi sifa ndogo na pia sipendi sifa bila ushahidi.Mimi ninachopenda kuona ni kwamba watu wote au wasanii wote waliopo katika hii tasnia ya Bongo Fleva wawe wanaumiza vichwa.Binafsi nathamini sana suala la kuumiza kichwa katika tungo na kazi zangu. Kwa hiyo kama kuna ambao wananiona mimi kama role model,basi la muhimu ni kufuata nyayo kwa kuumiza vichwa katika tungo zao na kazi zao kwa ujumla kabla hata hawajaingia studio.Binafsi namshukuru Mungu kwamba mpaka hivi sasa sijawahi kutengeneza wimbo ambao ukaishia studio tu.Namshukuru sana Mungu kwa hilo.

BC: Sasa hebu tuongelee kidogo kuhusu wimbo wako wa “Malumbano”… ambao ni miongoni mwa nyimbo zako zilizotokea kupendwa zaidi…ni wimbo wa mapenzi. Bahati mbaya au nzuri, Tanzania sasa hivi wasanii wengi wanapenda kuimba nyimbo za mapenzi. Unadhani ni kwanini wimbo ule,ingawa uko katika maudhui ambayo tunaweza kusema yameshazoeleka kupita kiasi, wenyewe umetokea kubamba zaidi?

20%: Kikubwa zaidi katika nyimbo ya Malumbano ni kwamba nimeongelea mazingira ambayo tunaweza kuita ni mapenzi.Lakini Ya Nini Malumbano ni neno ambalo linajibeba lenyewe,halimaanishi mapenzi peke yake.Maudhui ya wimbo ule yanaweza kutumika katika maeneo mengi..mfano hata barabarani hata ukiwa barabarani na gari yako mbovu na ukaona inataka kuzimika,ni vyema ukaliweka pembeni.Kwa busara unalisogeza pembeni na kupisha wengine.Hakuna haja ya malumbano.
Mfano mwingine unaweza kuwa na taaluma yako nzuri,unaingia kazini na unakuta eneo limetawaliwa na chuki na maneno maneno.Katika mazingira kama hayo mimi sioni kama kuna haja ya kuendelea kulumbana.Basi unaweza tu kujiweka pembeni kwani taaluma yako inabakia kichwani mwako.Mifano ipo mingi sana kuonyesha jinsi gani haina haja ya Malumbano ambayo ndio maudhui makubwa ya wimbo ule.

BC: Sasa hebu tuongelee kidogo masuala ya ubunifu kwamba unapokuwa studio yule producer wako anakupa uhuru wa kufanya unachotaka au kuna mtu/watu wanaokupa muongozo zaidi.Unapoingia studio huwa inakuwaje?

20%: Mimi binafsi huwa napenda sana kufanya kazi na producer ambaye ananipa pia muda wa kuzungumza na kuchangia katika uboreshaji wa kazi nzima kwa sababu mimi ninapotunga wimbo huwa natunga pia kila kitu mfano beats,chorus,mpangilio wa ala nk.Kwa hiyo huwa napenda kupata producer ambaye pia ananisikiliza.Nashukuru Mungu kwamba producers wangu ninaofanya nao kazi tunashirikiana vizuri kabisa katika kuhakikisha kwamba kitu kinachotoka ni katika kiwango cha kueleweka na kukubalika.

BC: Taarifa nilizonazo zinasema kwamba watu waliposikia umeshinda tuzo kibao, kuna sehemu inasemekana watu walishangalia kama tunavyoshangilia mpira. Unajisikia vipi ukisikia vitu kama hivi?

20%: Kwa kweli inatia moyo na kuleta raha sana kuona jinsi gani watu wanakubali kazi zangu. Na nasikia kelele hizo hazikuwa pale ukumbini tu bali sehemu zingine nyingi nchini Tanzania.Hiyo ni kumaanisha kwamba watu wengi walipenda ushindi ule utokee na walijitolea na kujituma katika kunipigia kura.Haishangazi kuona kwamba jina langu lilipokuwa linatajwa tu katika kategori fulani fulani,tayari watu walikuwa wanalipuka kwa kushangilia.
Napenda kuwashukuru sana mashabiki wangu na watanzania wote kwa ujumla kwa kuniwezesha kuibuka na ushindi huo.

BC: Sasa nini kinafuata baada ya hapa.Unaendelea na ziara zako,unajiandaa kufyatua album nyingine au mambo gani yanaendelea?

20%: Kusema kweli hapa nahitaji kuingia ofisini kumalizia movie yangu moja ninayofanya na ndugu yangu Afande Sele.Inaitwa Haki Iko Wapi? Baada ya hapo nitaendelea na kazi zangu zingine na pengine kama kutakuwa na Kili Music Awards Tour-maana mpaka hivi sasa bado sijapokea au kusikia chochote kuhusiana na kitu kama hicho. Zaidi ni kuendelea na kazi tu kama kawaida.

BC: Labda kwa kumalizia tu,una ushauri gani kwa vijana wanamuziki wenzako au wengine wanaoota kufikia mafanikio kama haya yako yaliyojidhihirisha kupitia Kili Music Awards.

20%: Ninachopenda kuwaambia neno la kwanza ni waandike sana.Na neno la pili waandike sana na hata neno la tatu pia waandike sana.

BC: Asante sana kwa muda wako 20%.Kila la kheri katika kazi zako

20%: Asante sana Bro.

Habari hii ni kwa hisani ya: BC EXCLUSIVE: MAHOJIANO NA 20% JUU YA USHINDI WAKE WA TUZO 5 ZA KILI MUSIC AWARDS 2011 - BongoCelebrity

Login to post comments

MSANII WA WIKI

Loveness

MUIGIZAJI na Mtayarishaji wa Filamu Tanzania Loveness Watson Nyota yake kwa sasa inatingisha katika tasnia ya

Soma Zaidi...

VIDEO YA MHARIRI

Off Side

Si mara ya kwanza kutazama filamu za Kanumba, lakini pia ni ukweli kwamba kila filamu anayokuja nayo

Soma Zaidi...

FILAMU ZA BONGO

Mbawa za Dino Zafunguka

MUIGIZAJI na Mtayarishaji wa filamu hapa nchini Tanzania Dennis Sweya (Dino) anatarajia kuanza kurekodi

Soma Zaidi...

WAHAPAHAPA VIDEO

You need Flash player 6+ and JavaScript enabled to view this video.