Jina la Usajili:  Neno la Siri:    Umesahau neno la siri?   |   Umesahau jina?
Administrator

Administrator

My name is sterling and this is my profile.

Tovuti/Blogu:

KARIBUNI sana wapenzi wasomaji wa safu hii ya ‘Vunja vunja’ ambayo hukupatia nafasi ya kujua kila kinachoendelea katika tasnia ya filamu ya nchini hapa.

Leo katika makala ya leo ningependa kutoa ushauri wa bure kwa wasanii wa Tanzania kuangalia suala la kufungua maduka ya kusambazia kazi zao.

Nimeamua kuandika hilo kwa sababu imekuwa kama kawaida kwa wasanii mbalimbali ikiwamo waigizaji wa filamu kulalamikia suala la wizi wa kazi zao.

Unapozungumzia suala la wizi za kazi za wasanii hili halipo hapa nchini pekee bali hata kwa wenzetu walioanza sanaa hizo kitambo ingawa wao hailingani na huku.

Nasema hivyo kutokana na wao kuweka sheria ambazo ni madhubuti zinazowabana wezi hawa na kuwafanya hata wale wanaojihusisha kuwa na woga.

Katika nchi zilizoendelea wamekuwa wakiithamini tasnia hii ya filamu kama moja ya sehemu ambazo zinatoa ajira kwa wananchi wake.

Ukiondoa hilo, pia serikali inajinufaisha kwa kujipatia kodi ya mapato hali ambayo inakuwa na tafsiri rahisi kuwa unapoichakachua kazi ya msanii ni sawa na kuiibia nchi mapato yake.

Kutokana na hilo, wananchi wake wamekuwa wakitambua fika wanapofanya mchezo wa wizi huwa wanakuwa na mashitaka mawili ya kukwepa mapato na wizi, hivyo wanajikuta wakipata tabu pindi wanapobainika.

Kwa hapa kwetu bado hata serikali yetu imekuwa ikichukulia suala la sanaa kama sehemu ya kujifurahisha na kuburudisha na sehemu ya ajira rasmi.

Sababu hiyo ndiyo hasa imefanya hata kushindwa kufikiria kutafuta mapato kupitia filamu au kulivalia njuga suala hilo la wezi wa jasho la wafanyakazi wa tasnia hii.

Kama serikali ingethamini michango yao wangekwenda mbali zaidi kwa kutetea masilahi yao kuliko kuwakaribisha bungeni ambako siku hizi pamepachikwa jina la utani la ‘Kariakoo’.

Sidhani kama msanii mwenye msimamo na anayefikiri sawasawa angekwenda pale na kufurahia kukaribishwa kula kipupwe cha kiyoyozi na watu ambao wanashindwa kuwasaidia kutungwa sheria kali za kuzia wizi wa kazi zao ili wao waweze kufaidika na jasho lao.

Nilisikitika pindi nilipokuwa nikiwaona waheshimiwa hawa wa mjengoni walipokuwa wakiwapaka wasanii wetu mafuta kwa mgongo wa chupa kwa baadhi yao wakitaka kupiga nao picha huku wakijua fika wameshindwa kabisa kuwasaidia kilio chao cha kuwahakikishia wanatambua ajira yao na kuwa rasmi ili kila anayekamatwa kwa wizi atakutana na sheria kali itakayomfanya awe mfano kwa wengine.

Hata kama wahusika watakuwa hawataki kuitambua kama ajira rasmi wangeweza kubadili sheria za zamani za kupigwa faini zisizokidhi na wakati wa sasa ambazo zinaonekana ni adhabu uchwara ukilinganisha na fedha anazokuwa amezichuma.

Kiasi cha faini ambacho kinalipishwa ni aibu kusema kwa kuwa naamini nikikiweka hapa naweza kuzalisha kundi jingine kubwa la wezi wa kazi hizo wakiamini wanao uwezo wa kulipa faini hiyo.

Leo tuishie hapa, karibu wiki ijayo utambue dawa ambayo itawasaidia wasanii wenyewe pasipo kuwategemea zaidi hawa watawala wetu ambao wanaonyesha dhahiri kutoithamini tasnia hiyo.

na Shabani Matutu

AHLAN wasahlan mpenzi msomaji wa safu hii ya Jamvi la Kulonga ikiwa ni Ijumaa nyingine tunapokutana kwa lengo la kuchambua na kujadili hili na lile lililojiri katika anga ya burudani na sanaa kwa ujumla.

Leo katika Jamvi hili ningependa kuzungumzia hatua ya Kampuni ya Aset ya jijini Dar es Salaam chini ya mwanamama Asha Baraka ‘Iron Lady’ kuamua kuandaa onyesho maalumu la kukusanya fedha kwa ajili ya kuchangia matibabu ya gwiji la muziki wa dansi nchini, Muhidin Maalim Gurumo, maarufu kwa majina ya ‘Mzee wa Masaki’ au ‘Uncle Gurumo’ ambaye kwa miezi kadhaa amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa mapafu kujaa maji ambapo alilazimika kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kufanyiwa operesheni lakini bado hali yake kiafya haijakaa vema.

Katika onyesho hilo ambalo lilifanyika katika Ukumbi wa Mango Garden, Aset iliandaa onyesho hilo ambalo liliishirikisha bendi kongwe ya muziki wa dansi nchini ya Msondo Ngoma ambayo kiongozi wake ni Uncle Gurumo japo kwa sasa amejiweka kando katika kuitumikia bendi hiyo kutokana na maradhi yanayomkabili.

Jamvi la Kulonga likiwa mmoja wa wadau wakubwa wa muziki nchini limeguswa na hatua ya Aset kuona umuhimu wa kuchangia matibabu ya mzee huyo ambaye ameweka rekodi ya kudumu katika uimbaji kwa muda mrefu lakini kubwa zaidi akiwa na sauti ileile iliyojaa ubora ambayo alianza nayo tangu mwaka 1950.

Katika maelezo yake kwa Jamvi hili, Asha, anasema onyesho hilo lililenga kutunisha mfuko wa matibabu ya gwiji huyo, ambaye ametoa mchango mkubwa katika mafanikio ya muziki wa dansi, hivyo kuona umuhimu wa kumsaidia aweze kupona kwa sababu wanamuziki wengi hawana kipato cha kutosha lakini pia hawana pensheni baada ya kustaafu.

Katika onyesho hilo wadau waliweza kuchangia zaidi ya shilingi milioni 2 taslimu, mbali ya fedha zilizopatikana kutokana na viingilio vya waliohudhuria ambazo kwa mujibu wa Asha atakabidhiwa Gurumo ili ziweze kumsaidia katika kujitibu maradhi yanayomkabili ili aweze kurudi katika hali yake njema kiafya.

Mzee huyo aliwapagawisha mashabiki katika onyesho hilo pale alipopanda jukwaani kuwasalimia na kuamua kuimba wimbo mmoja ambapo kila aliyemsikia akiimba wimbo wa ‘Piga Ua Talaka Utatoa’ alishindwa kujizuia kukaa na kujikuta akimtunza Gurumo.

Nikirudi katika hoja ya msingi ni kwamba kitendo kilichofanywa na Aset kimelisukuma Jamvi hili kumpongeza Asha Baraka kwa uamuzi wa kampuni yake kuonyesha kujali afya ya Gurumo, jambo ambalo linapaswa kuigwa na bendi nyingine katika kusaidiana wanamuziki na kushauri kuwa isiishie katika maradhi pekee, kwani yako matatizo mengi yanayowakabili wanamuziki na yakiwa yameshindwa kupatiwa ufumbuzi.

Unapouzungumzia muziki wa dansi nchini wa enzi na enzi ni lazima utaje jina lake kutokana na kushiriki kuanzisha bendi mbalimbali za muziki huo tangu mwaka 1961 ambapo alishiriki kuimba nyimbo mbalimbali za kuhamasisha masuala mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Jamvi hili linakumbuka mchango wa Gurumo katika kushiriki kuasisi bendi kongwe ya muziki wa dansi ya NUTTA Jazz ambayo bado yupo nayo hadi leo ikiwa imepitia majina mbalimbali ya JUWATA Jazz, OTTU Jazz na sasa ikiitwa Msondo Ngoma Music.

Miongoni mwa wanamuziki wakongwe ambao wameuletea mafaniko muziki wa dansi nchini ni Gurumo, ambaye mpaka sasa anajivunia kuona bendi zote alizoshiriki kuzianzisha zimeendelea kuwepo katika medani ya muziki tena kwa mafanikio lakini na
yeye akiwa bado ana uwezo wa kuimba. Ni mmoja wa wanamuziki walioshiriki kuanzisha NUTTA Jazz ambayo kwa sasa inaitwa Msondo Ngoma mwanzoni mwa miaka ya 1964, lakini pia akiwa ni mwanzilishi wa DDC Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’ iliyoasisiwa 1978 akiwa na wapiga solo Abel Baltazar na Joseph Mulenga na nguli Hassan Rehani Bitchuka na wengineo.

Tungo zake alizowahi kutunga na anazoendelea kutunga akiwa na Msondo Ngoma ni dhahiri zimeendelea kutesa na kumuongezea heshima kutokana ujumbe uliomo katika kuielimisha jamii na kusaidia wakati huo katika harakati za mapambano ya kupigania uhuru kwa nchi ya Msumbiji ambapo aliweza kutunga wimbo wa ‘Viva Flerimo’. Kuugua kwake ni pengo kubwa kwa wadau wa muziki huo kwani damu changa zilizopo Msondo Ngoma zinahitaji kurithishwa mikoba ya kujua maadili ya muziki na thamani ya mwanamuziki katika kutunga na kuimba ili nyota yake izidi kung’ara.

Gurumo ni mwanamuziki mtunzi, mwimbaji mkongwe na mbunifu wa mitindo mbalimbali ya dansi kama vile ‘Msondo Ngoma’, ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’ (alipokuwa Mlimani Park) na Ndekule (alipohamia kwa muda Orchestra Safari Sound Wana OSS) akiwa na Hassan Rehani Bitchuka na Skasy Kasambula. Lakini sifa na heshima kubwa aliyonayo Uncle Gurumo ni kushiriki kuasisi bendi hizo pamoja na mtindo ambapo akiwa na NUTTA Jazz ndiye aliyeanzisha mtindo wa ‘Msondo Ngoma’ na alipokwenda kuiasisi DDC Mlimani Park aliasisi mtindo wa ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’, ambayo imeendelea kutumiwa na bendi hizo hadi leo.

Akiwa na bendi hiyo ya Nuta Jazz, Gurumo alitunga nyimbo nyingi ambazo ni ‘Magdalena’, ‘Maneno ya Mwalimu’, ‘Maneno ya Wazee Yote Sawa’, ‘Rehema Umefeli Shule kwa Kisa Gani’? na nyinginezo. Baadaye bendi hiyo ilibadilishwa jina na kuitwa Jumuiya ya Wafanyakazi, JUWATA, ambapo akiwa na bendi hiyo baadhi ya vibao alivyotunga ni ‘Dada Fatuma’, ‘Dada Sabina’ kabla haijabadilishwa na kuwa OTTU Jazz Band ambapo moja ya nyimbo alizotunga na kumpatia umaarufu ni ‘Usia wa Baba’ lakini akiwa alitunga ‘Majuto’. Jamvi la Kulonga linatambua na kumheshimu mzee huyu kutokana na ubora wa sauti aliyonayo ileile tangu enzi za NUTTA lakini nilipowahi kuumuliza siri ya mafanikio alibainisha kuwa ni kutojihusisha kwake na ulevi na anasa zingine za dunia, vitu ambavyo ni sumu kwa mwanamuziki.

Mwanamuziki huyo alizaliwa Masaki, Kisarawe mwaka 1940 na kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Sungwi huko huko Kisarawe, na baadaye aliacha shule baada ya baba yeke kufariki dunia na kukosa mtu wa kumgharamia mahitaji ya shule. Baada ya kuacha shule kutokana na kufiwa na baba yake, Gurumo mwaka huo huo alijiunga na bendi ya mtaani iliyojulikana kama Scock Jazz iliyokuwa na maskani yake katika mitaa ya Moshi na Kigoma.

Mwaka mmoja baadaye alijiunga na bendi ambayo ilikuwa na vyombo vya kisasa wakati huo, iliyojulikana kama Kilimanjaro Chacha, ambako alitunga vibao kama vile ‘Twende Tukalime’, ‘Mapenzi Hayana Dawa’, ‘Ushirikina ni Sumu ya Maendeleo’. Mwaka 1963 Gurumo alijiunga na Rufiji Jazz Band, ambako alitunga kibao cha ‘Uwezo wa Binadamu Kufikiri’, ambacho kilimpatia umaarufu mkubwa kufuatia kupendwa na wapenzi wengi wa muziki wa dansi. Baadaye mwaka huo huo alijiunga na bendi ya Kilwa Jazz na kutunga kibao cha ‘Wewe Mpenzi Naomba Unishauri Kabla Hatujagombana’, na kile cha ‘Siwezi Kukununulia Gari Wakati Hata Baiskeli Sina’.

Mwaka 1964 alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa bendi ya Nuta Jazz, akiwa na kina Mabruki Khalfan, Ahmed Omary, Mohamed Omary, Epimakus Mkundika na Rashid Abdallah. Jamvi la Kulonga linamuombea kwa Mwenyezi Mungu ‘Uncle’ Gurumo aweze kupona kwa haraka na kurejea jukwaani japo ameshafanya uamuzi wa kustaafu lakini bado wadau tunahitaji kusikia ladha ya sauti yake, kuendelea kuwaburudisha wapenzi na mashabiki wa bendi ya Msondo Ngoma na wadau wa muziki wa dansi.

MWANAMUZIKI mahiri wa miondoko ya Hip hop ambaye pia ni muigizaji wa Filamu kutoka nchini Marekani ajulikanae kwa jina la Christopher Brian Bridges ‘Ludacris’ anatarajiwa kutoa shoo ya aina yake kesho katika kilele cha Tamasha la Serengeti Fiesta 2011, litakalofanyika kwenye Uwanja wa Leaders Club Dar es Salaam.

Akizungumza jana na Tanzania Daima Mkurugenzi wa Maendeleo na Utafiti wa Kampuni ya Clouds Media Group, Ruge Mutahaba anasema taratibu zote za kumlela Ludacriss zimekamilika hivyo Watanzania wakae mkao wa kupata raha ifikapo kesho.

Likiwa linafanyika kwa mara ya kumi sasa tamasha hili linakwenda kwa jina la Serengeti Fiesta 2011 na linatarajiwa kuwa na msisimko wa aina yake ambapo katika miaka yote hiyo ya nyuma kufanyika wasanii mbalimbali wa kimataifa waliweza kutumbuiza.

Kwa mwaka jana alikuja Lil Kim ambapo alikonga nyoyo za mashabiki katika tamasha hilo lililofanyika Leaderds Club, wasanii wengine waliowahi kuja ni pamoja na Jarule na Koffie Olomide.

Aidha, katika kusherehekea miaka kumi ya Serengeti Fiesta 2011, uzinduzi wa tamasha la mwaka huu alikuja msanii wa kimataifa Shaggy, ambapo pia kwa mara ya kwanza lilizinduliwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Uzinduzi huo wa kufana ulijawa na mambo mengi mazuri ikiwa ni pamoja na Shaggy kuweza kutembelea nyumba ya asili ya Wasukuma katika sherehe za msimu wa mavuno ‘Bogobogo’ na baadaye alifanya shoo ya aina yake na iliyoacha gumzo pale CCM Kirumba .

Ruge anasema kwamba shamrashamra za kufikia kilele cha miaka 10 ya Serengeti Fiesta 2011 kwa mwaka huu zimekuwa tofauti na zenye msisimko mkubwa ikilinganishwa na miaka mingine yote iliyowahi kufanyika tamasha hilo.

Ikumbukwe kwamba kabla ya kuzinduliwa Serengeti Fiesta kulifanyika matamasha kadhaa ya amshaamsha ambayo ni pamoja na Serengeti Fiesta Soka Bonanza, Serengeti Freestyle, Serengeti Dansi la Fiesta na Serengeti Filamu Fiesta, mchakato uliofanyika katika mikoa kadhaa, ambapo washindi wake waliopatikana na vipaji lukuki kuvumbuliwa wameweza kuingia mkataba wa kusaidia kuendelezwa katika tasnia husika.

Mutahaba anasema kwamba milango ya Leaders itakuwa wazi kuanzia mchana hadi usiku ambapo mtu akinunua tiketi kabla ya onyesho ni sh10,000 na mlangoni atachajiwa kiasi cha sh15,000.

Tamasha hilo limeratibiwa na Kampuni ya Prime Time Promotiona kwa ushirikiano na Clouds Media Group na mdhamini mkuu akiwa ni Kampuni ya Bia ya Serengeti.

Aidha, Mutahaba anatoa shukurani za dhati kwa niaba ya wadhamini na kampuni anayoiwakilisha kwa wakazi wa mikoa yote ambayo tamasha hilo la Serengeti Fiesta limekwishafanyika, kwa kuitikia wito na kujitokeza kwao kwa wingi kwani imedhihirisha jinsi tamasha hilo linalowakutanisha watu wa aina na rika mbalimbali linavyowajengea upendo wa umoja na mambo mengine mbalimbali ikiwamo kufahamiana.

“Fiesta ya mwaka huu tumepata sapoti kubwa kutoka kila kona nchini ambako tulifika kwa asilimia kubwa, hivyo hatuna budi kulishukuru Jeshi la Polisi Tanzania kwa kutupa ulinzi wa kutoka kila mahali tulipokwenda, zikiwemo na halmashauri za miji yote kwani zote zilizoshiriki kwa namna moja ama nyingine zimesaidia kulifanikisha tamasha la Serengeti Fiesta 2011,” anasema Mutahaba.

“Kadhalika nawashukuru wasaniii wote walioshiriki kwenye matamasha yaliyofanyika kwenye mikoa yote kwa ujumla wao na vyombo vyote vya habari kwa pamoja nadhani tuko pamoja katika kuijenga Fiesta 2011.

na Khadija Kalili

KATIKA taratibu za kusaka vipaji na kuendeleza vipaji vya muziki wa dansi ya kizazi kipya, kupitia Kampuni ya Benchmark Productions, kuna changamoto kadhaa kutokana na uendeshaji wa shindano hilo.

Changamoto inayokera taratibu za shindano hilo ni pamoja na utaratibu wa majaji ambao ndio waamuzi wa kumpata mshindi wa shindano hilo.

Mara nyingi sehemu wanapokutana majaji kwa ajili ya shindano fulani, wadau huongeza umakini kwa kuyafuatilia mashindano yanayofanyika ambayo wanatakiwa kuyatolea uamuzi.

Lakini Bongo Star Search (BSS) ina ukakasi katika majaji, tatizo ambalo linatishia kuwafukuza wadau na wapenzi wanaofuatilia shindano hilo ambalo ni bora zaidi Afrika Mashariki na Kati.

Tanzania Daima ni taasisi inayoshirikiana na wadau wengine wa maendeleo ya sanaa kama ya Madam Rita, ambaye alifikiria kuandaa shindano ambalo litawakomboa wadau wengi wa sanaa na jamii kwa ujumla.

Uozo unaoitawala BSS ni pamoja na matamshi ambayo yanawakatisha tamaa washiriki na kujiona kwamba hawawezi kufanya sanaa kwa mara nyingine, sambamba na lugha mbovu ya majaji ambao wanatakiwa kuwa na mwongozo bora utakaokuwa mfano kwa jamii kuliko wanavyofanya, jamii ya Tanzania haielewi kinachofanyika.

Hongera Baraza la Sanaa (BASATA) kwa kufikiria kuwa na mrejesho wa matukio ya sanaa, ikiwa BSS ni tukio la tatu kufanyiwa mrejesho baada ya Kisura, yaliyofanyiwa mrejesho wiki iliyopita.

Wadau wamependekeza kama inawezekana wawapangue majaji wanaotoa mshindi wa BSS, kwa sababu vituko vinavyofanywa na majaji hao si mwenendo wa mila na desturi za Kitanzania ama kama inawezekana wajaribu kuwashawishi Watanzania kuhusu kile wanachokifanya kuliko kuwalazimisha jambo ambalo hawalielewi.

Utetezi wa Madam Rita ni kwamba zile ni changamoto za sanaa na akakubali kwamba matendo yanayofanywa na majaji wake atayafanyia kazi, kwa sababu yanawakera wengi, ingawa akasema hatabadili majaji wake ila atatoa semina kwa majaji wake.

Ni shindano bora kati ya mashindano ya kusaka vipaji Afrika Mashariki na Kati, lakini linapotezwa na majaji ambao hawajapata mwongozo ambao utafanikisha maendeleo ya sanaa.

Kwa sababu Madam Rita amezikubali changamoto hizo, inabidi azingatie ipasavyo, kwa sababu shindano hilo linatazamwa na wadau mbalimbali wakiwamo watoto ambao wanahitaji kujifunza kupitia BSS, ikiwa masuala yenyewe ndiyo kama yanavyofanywa na majaji hao.

Wadau wengine wanaolitazama shindano hilo ni pamoja na wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mataifa mengine yanayofuatilia sanaa za nchi mbalimbali.

Kila lenye ubora lina matatizo yake, Madam Rita pokea mapendekezo ya wadau ili upige hatua zaidi ya ulipo sasa, badilika ili kufanikisha malengo yako.

Wanamuziki wote wa Kiafrika duniani kote. Huu ni mwisho wa wito kwa wasanii wanaotaka kushiriki katika tamasha la Sauti za Busara 2012. Jopo la uchaguzi litakutana mnamo mwezi wa nane kuchagua wasanii watakaoshiriki katika tamasha la mwakani 2012. Ili maombi yako yaweze kushughulikiwa ni lazima tupokee nakala moja au mbili ya kazi yako ya hivi karibuni (CD au DVD), picha pamoja na maelezo ya kikundi. Tuma maombi yako kabla ya tarehe 31 Julai 2011

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunzinza hivi karibuni alimtumia ujumbe mwigizaji maarufu wa filamu Bongo, Irene Uwoya (pichani) akimtaka aende Ikulu kwake kwa ajili ya mazungumzo, Amani lina habari kamili.

Akizungumza na mwandishi wetu Julai 25, mwaka huu, Uwoya alisema Rais Nkurunzinza alimuita baada ya kusikia kuwa yupo nchini kwake na amevuta hisia za wengi.

“Nilipokwenda Burundi kwa ziara ya kisanii Rais Nkurunzinza alipata taarifa, akaambiwa nimeitingisha sana nchi yake. Kutokana na taarifa hizo alitaka kuniona, akanitumia gari na ulinzi wa polisi ili waje kunichukua.

“Kwa kuwa sikuwa na muda mrefu wa kukaa Burundi kufuatia kutakiwa kurudi haraka Cyprus kwa mume wangu, ilibidi nikatae,” alisema Uwoya.

Akaongeza kuwa, licha ya kipindi hicho kushindwa kuonana na rais huyo, bado amekuwa akiendelea kumsihi atafute siku amtembelee hivyo ameamua kutimiza hilo atakapoacha kumnyonyesha mwanaye.

“Sikuwahi kuwaza kama kuna siku ningeweza kwenda nchi yoyote na kukusanya umati mkubwa wa watu kiasi kile, pia sikuwahi kuota kama siku moja ningeweza kuwa staa wa kuombwa kukutana na kiongozi maarufu wa nchi yoyote kama ilivyotokea kwa Rais wa Burundi.

“Kwa sasa bado najipanga, nitaenda kuonana naye pindi mwanangu atakapoacha kunyonya kwani ni bahati kwangu kukutana na kiongozi huyo kupitia kazi zangu za kisanii,” alisema Uwoya.

Msanii Khalfan Ilunga ambaye anajulikana zaidi kama Cpwaa amefanikiwa kuwa msanii wa kwanza wa kitanzania kupata nafasi ya kupiga shoo katika fainali ya Big Brother Amplified 2011.     Msanii huyo Cpwaa anatarajiwa kupiga shoo katika fainali hizo pamoja na waimbaji wengine maarufu wa kitanzania ambao,

nipamoja na Fally Ipupa (DRC-Congo),wizkid na Mo Cheddah (Nigeria),Professor na Speedy wa Afrika Kusini.

katika taarifa kwa vyombo vya habari waandaaji wamesema show hiyo ya fainali ya Big Brother Amplified 2011 ambayo imejizolea umaarufu mkubwa pamoja na sherehe ya fainali ambapo mshindi atajinyakulia kiasi cha dola za kimarekani laki mbili pia itawajumuisha wasanii hao sita wa kiafrika pamoja na washiriki  wote waliotoka mapema.

katika taarifa hiyo kwa vyombo vya habari mkurugenzi wa Mnet Africa bwana Biola Alabiamesema "tutawapagawisha mashabiki wa shindano hili kwa kuwashtua na zawadi kubwa kabisa ambayo haijawahi kutokea katika shindano hili.

Najua mashabiki mtakuwa mnafahamu hivyo lakini washiriki waliomo ndani ya jumba la BBA Amplified hawajui kama kutakuwa na zawadi mbili za dola laki mbilimbili hivyo inatarajiwa kuleta mshtuko na hamasa kwa washiriki na watazamaji.

wakati huo huo shindano la mwaka huu la Big Brother Amplified 2011 limevunja rekodi ya wingi wa meseji kwa kupata jumla ya kura milioni 1 na laki 4 kwa wiki ya jana tu hivyo kufanya jumla ya idadi ya kura zote zilizopigwa kufikia milioni 6 na laki 3 na kuwa idadi kubwa zaidi ya kura katika mashindano yote ya Big Brother yaliyopita hivyo waandaaji wamewataka wapenzi wa shindano hilo kuendelea kupiga kura kwa wingi katika siku chache zilizosalia.

MSANII nyota katika tasnia ya filamu Zuwena Mohamed aka Shilole ameiambia FC kuwa katika filamu ya Tifu la Mwaka amekamua vilivyo na kuonyesha kiwango cha hali ya juu katika filamu hiyo, Tifu la mwaka ni filamu iliyoandaliwa na Issa Mussa almaarufu kama Cloud 112, filamu hii tayari imemalizika katika kurekodiwa na ipo katika hatua za uhariri kufuatia maelezo ya msanii huyu anaamini kuwa ni filamu bomba.

“Nimecheza katika kiwango cha hali ya juu sana katika filamu hii ya Cloud nawaahidi wapenzi wa filamu kuwa kila siku nazidi kupanda na hasa ukizingatia kuwa kwa sasa nahisi katika uigizaji kwa upande wa akina Dada naweza kuwa sina mpinzani, napiga kazi na kwa kuonyesha hilo wasikose kuangalia filamu ya Tifu la Mwaka ni tifu kweli, hapa unaweza kupima uwezo wa watu” Analonga Shilole.

Mwanadada huyu ambaye ni mjasirimali anayemiliki Pub yake mitaa ya Mwananyamala Komakoma amekuwa gumzo katika tasnia ya filamu baada ya kushiriki katika filamu kadhaa ni msanii anayejiamini kwa kile anachofanya, katika filamu hii ya Tifu la Mwaka imeshirikisha wasanii kama Issa Mussa (Cloud 112), Baby Madaha, Suleiman Barafu, Ummy Wenslaus (Dokii), Zuwena Mohamed (Sholole).

MWANAMUZIKI wa muziki wa kizazi kipya nchini, na mkali wa staili ya kiduku Marlaw anatarajia kufanya Tour katika nchi za  bara la Ulaya kwa kufanya show katika nchi tano za bara hilo, ambapo ataondoka siku ya jumanne julai 26.

Mwanamuziki huyo nchi ambazo anategemea kwenda kufanya show, kwa kuwafundisha staili ya kiduku ni Ufaransa, Uholanzi, Norway, Uswisi na Ujerumani.

Toka maskani ya TipTop Connection DHW inataarifiwa kuwa Rapper Abdul a.k.a Dogo Janja yuko studio akigonga track mpya inayokwenda kwa jina la 'Siri zao'.

Katika track hiyo Dogo Janja amempa shavu mkali toka pande za TMK namzungumzia Chegge Chigunda mtoto wa Mama Saidi.

<< Mwanzo < Iliyopita 1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 Inayofuata > Mwisho >>
Page 1 of 29

MSANII WA WIKI

Loveness

MUIGIZAJI na Mtayarishaji wa Filamu Tanzania Loveness Watson Nyota yake kwa sasa inatingisha katika tasnia ya

Soma Zaidi...

VIDEO YA MHARIRI

Off Side

Si mara ya kwanza kutazama filamu za Kanumba, lakini pia ni ukweli kwamba kila filamu anayokuja nayo

Soma Zaidi...

FILAMU ZA BONGO

Mbawa za Dino Zafunguka

MUIGIZAJI na Mtayarishaji wa filamu hapa nchini Tanzania Dennis Sweya (Dino) anatarajia kuanza kurekodi

Soma Zaidi...

WAHAPAHAPA VIDEO

You need Flash player 6+ and JavaScript enabled to view this video.