Utangulizi Print
04 Aprili 2010

UtanguliziWAHAPAHAPA ni mchezo wa radio wenye nia ya kubadili mtazamo wa kimaisha kuwa chanya. Mchezo huu unalenga suala zima la mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, matibabu na uangalizi.

Mchezo huu unarushwa kila wiki kwa namna ya kuvutia na kuelimisha, kwa njia ya mawasiliano ya radio.

Maisha yanayojiri katika mchezo huu yanatokea katika vijiji vya kufikirika vya KALUMBI na MAKATANI vilivyoko sehemu Fulani huko Tanzania.

Wahapahapa Studios“Homeboys” ni bendi ya muziki ambayo ndio kiunganishi cha matukio yote yanayojiri katika mchezo huu wa kusisimua. Bendi hii inaundwa na wavulana watano ambao baadae kidogo mwanamuziki wa kike anajiunga nao.

Bendi hii inaamini kuwa ikipiga muziki mzuri itafanikiwa kimaisha na hatimae watakuwa nyota kwa washabiki wao wa nyumbani. Bendi inakutana na changamoto kadhaa zinazokinzana na nia yao ya kuwa vinara wa muziki pamoja na kujitengenezea kipato. Kuna migogoro lakini haikosi suluhisho, maslahi ya bendi ni makubwa zaidi ya maslahi ya mtu mmoja mmoja.

Hatuishii kuona maisha ya wanabendi peke yake bali mchezo unazidi kunoga zaidi pale tunapokaribishwa kuona pia maisha ya ndugu, familia, jamaa, na marafiki wa wanabendi. Tunaona migogo na changamoto inayokabili jamii hii na jinsi inavyoamua kuungana pamoja kupambana kuelekea siku mpya.